MAISHA KWENYE UMWALI

Naam, pandashuka za maisha hayana mwisho. Hivi majuzi tumekuwa vema maisha yakiendelea bila tashwishi yoyote lakini leo twaishi kwa hofu maana hatujui nini yatungoja hapo mbeleni. Lakini, si ni desturi tu maisha lazima yaendelee kwa neema zake Mola? Ama kweli maisha kitendawili, jibu unalo. Habari za kusitikisha zilitupata tuliposkia mlipuko wa virusi vya Corona zinapoaminika kuwaathiri wachina mwanzo kabla ya kuenea dunia nzima. Idadi ya waambukizwa wa virusi vya Corona kuongezeka kila siku na idadi ya wafu ililazimu serikali nyingi kusitisha shughuli za kawaida. Uamuzi huu umewaathiri watu katika shughuli mbali mbali.


Namna vitu vilivyobadilika kwa upesi ni ya kustaajabisha kweli. Binadamu kuishi kwa uoga kwa sababu ya janga hili lililotupata kutokana na kuenea kwa virusi vya Corona. Wachanga kwa watu wazima, wote hawana amani swali ikiwa, ‘ Ni lini maisha ya zama yatarejea’ Wasafiri kupewa uhuru wa kusafiri,wanabiashara kupata fursa ya kubobea katika eneo lao,wanagenzi haswa watahiniwa kurejea shuleni na matumaini ya kuufanya mtihani wa kitaifa, haya yote yamesitishwa kwa sababu ya virusi vya Corona. Wavyele nyumbani hawana yeyote wa kusikiza dua lao kwa sababu hali ya maisha si nzuri kamwe. Hawajui watakapopata riziki ili waweze kuwalisha watoto wao. Nani wa kulaumiwa?

Hamna, ila ni masaibu yanayojiri kila kunapokucha. Wazazi wanatamani angalau shule zingefunguliwa hivyo wawe na amani kuwa watoto wao wamepata kitu cha kutia tumboni lakini, ni mzazi yupi ataweza tia mwanake hatarani? Hivyo basi, wanaona heri wawe pamoja hata kama chakula ni nadra. Matumaini yao ikiwa, siku moja haya masaibu yatakuwa tu kisa cha kusimuliwa siku za usoni.


Habari tunazopata mara kwa mara, ni visa vya kusitikisha mno. Vifo vya watoto kutokana na njaa. Kisa cha mama mmoja aliyewapikia wanawe mawe, ilivunja nyonyo za watu wengi. Lakini, mbona maisha ngumu hivi? Wana kulilia nina yao ‘Mama tupe chakula, mama twahisi njaa mama ..’ Ama kweli uchungu wa mwana ajuaye ni mzazi. Na lisilo budi hubidi. Mama huyo alitiwa majonzi kwa sababu hapakuwa na chakula cha kuwapa wanawe lakini kama mama, hakutaka kuwavunja nyonyo zao hivyo basi akaamua kuwatapeli kwa kuyachemsha mawe ili wadhani kuwa mama alikuwa anawaandalia chakula.

Machozi tele yanatiririka ninaposimulia kisa hiki kwa maana baada ya siku kadhaa mama huyu kampoteza mwanawe mchanga wa miezi mitano tu! Jameni, laiti angepata msaada mapema, leo hivyo mwanawe angekuwa hai. Huu ni mfano mmoja tu lakini ukweli ni kuwa watu wengi wanaangamia kutokana na janga hili.


Ukweli wa mambo ni kuwa sote hatuna maelezo maalum kuhusu ni lini swala hili litapitwa na wakati. Kile tunachoomba ni kuwa Maulana atuwie radhi na kutuondolea jinamizi hili. Tumewapoteza wapendwa wetu, jamaa zetu, marafiki zetu Ama kweli dunia nzima imeathirika. Nchi za ulaya licha ya kuwa na vifaa vya hospitali ya kisasa,wangali wanakabiliana na ugonjwa huu. Njia salama ya kujikinga ni kuhakikisha mtu ameepuka maeneo yaliyo na umati wa watu. Njia nyingine ni kunawa mikono kila mara kwa kutumia maji na sabuni kwa wale wanawezamudu kununua glavu na cha muhimu pia kuvaa barakoa usoni. Hivi basi anawezajikinga haswa mtu anapokuwa miongoni mwa watu wengi. Watu pia wanahimizwa kuepukana na umati wa watu, kusalimiana kwa mikono, kukumbatiana na kadhalika. Mikakati hizo zote zimeandaliwa na wizara ya afya ili kusaidia umma kujikinga dhidi ya virusi vya Corona.


Ni kweli kuwa sote tumeathirika lakini wengi wetu wanapuuza maagizo ambayo wizara ya afya imeandaa katika juhudi za kupunguza idadi ya waambukizwa wa Corona. Wengi wanalia kwa sababu wanakumbwa na njaa, wengine bado hawaamini huu ugonjwa si uzaha. Lakini, utawalaumu wale wanaokiuka sheria kwa sababu wapendwa wao wanakabiliana na ukosefu wa chakula? Hivi kidogo wanajipata katika ugumu, wafe nyumbani ama wajitose hatarini katika pilkapilka za kutafuta riziki. Imekuwa takriban miezi mitatu na wiki kadhaa tangu kusitishwa katika shughuli za kawaida, maisha yazidi kuwa ngumu ukosefu wa pesa ya matumizi na kupandishwa kwa bei ya bidhaa ikitia umma bughudha. Umma unajipata katika hali ya kukubali kuwa virusi vya Coronau ni Mola tu ndiye anayetulinda kwa wema wake la sivyo, sote tu wasafiri hakuna anayejua wakati wake utakapowadia.


Sekta tofauti zimeathirika kutoka sekta ya elimu, biashara, utalii na kadhalika. Watu wengi wamelazimishwa kuacha maeneo yao ya kazi kwa sababu ya kusitishwa katika shughul za kawaida, hivi basi uchumi pia umeathirika pakubwa. Ombi la kila mtu ni kuwa hali itarejea ilivyokuwa hapo awali. Wanafuzi waelekee zao shuleni wazazi nao waelekee kazini kusaka hela ya matumizi ya kukimu aila zao. Wengi pia wataweza kuwatembelea wapendwa wao ambao hawajawaona kwa muda mrefu tangu uhuru wa kusafiri kusitishwa. Mpaka wakati huu ombi letu ni Mola tupe chakula cha kila siku, tupe afya njema na utulinde tusiangamie . Wanasayansi wanashinda maabarani katika juhudi za kutafuta chanjo ya virusi vya Corona.Tuna matumaini kuwa juhudi zao zitazaa matunda na mwishowe wapate chanjo . Wakati huo huo tuwe waangalifu tusije tukalaumu yeyote kuwa hatukuonywa.

Muhimu tusisahau kusafisha mikono yetu kila wakati na mikakati zote wizara ya afya imetuandalia. Tuwe na imani haya yote yatapitwa na wakati ila kwa sasa tujikinge sote.
Kwa familia ambazo wamepoteza wapendwa wao, tunawaombea kwa wale wameathirika tunawaombea wapate nafuu. Kwa wale wenye hofu kwamba wanaonyesha dalili za kuwa na virusi hivi, tunawasihi wasitie shaka na waweze kutembelea daktari ile wapate kupimwa ili wajue hali yao. Kumbuka, kuvunjika kwa mwiko sio mwisho wa kupika ugali. Licha ya hali iliyotukumba maisha bado itaendelea. Tafadhali tuzingatie maagizo ambayo yameandaliwa na wizara ya afya ili tupunguze uwezekano wa kuambukizwa virusi hivi. Jameni tuoshe mikono kila wakati tukitumia sabuni. Epuka virusi vya Corona! Zingatia mikakati ya wizara ya afya na ya muhimu, sote tuwe salama!

A teacher, blogger, writer. Managing Editor of The Youthing Magazine. Life is beautiful.

You may also like...