RAFIKI

Katika enzi hizi, ni vigumu mno mtu kujielewa bila kuhusisha ndugu au mwandani. Pilkapilka za maisha ya sasa haziruhusu kamwe insi kujitambua kirahisi bila jamii.

Itapataje maana nafsi yake eti anajulikana kama mja akosaye mahusiano yoyote ile. Upweke ni uvundo. Hapo hawakukosea hata kidogo.

Binadamu anavyoendelea kukua, anapewa wosia wa kutangamana na watu ili awe mtu kamili. Mazingira yake nayo ni motisha tosha ya kujuana na watu wa muonekano na hulka ainati.

Rafiki ni nani? Sahibu ni mtu anayekufaa wakati wa furaha na majonzi. Ni nguzo nzito na dhabiti katika jamii kwa jumla. Urafiki ni ukuzaji wa familia, kijiji, kampuni, kiwanda na hali kadhalika.

Aisifuye mvua, imemnyea. Marafiki wamenifaa mimi haswa katika nyanja mbali mbali. Nimeweza kuona maana ya udugu na kusherehekea matunda ya mti huu nilioukuza kwa subira ivutayo kheri.

Urafiki ni imani, uaminifu matumaini, taadhima, ibada na kikubwa zaidi, urafiki ni UPENDO.

Rafiki hodari aanze na wewe.

You may also like...